Vodacom Tanzania imetangaza kuandaa mashindano ya baiskeli ambayo yatafanyika Jijini Mwanza mwezi ujao na yatagharimu zaidi ya shilingi milioni 50.
Akizungumza naWaandishi wa Habari, Jijini leo, katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Mkuu wa Udhamini wa Vodacom Tanzania, George Rwehumbiza alisema kwamba mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na kuwaomba waendesha baiskeli kujitokeza kwa wingi.
“Mashindano haya yameboreshwa kwa upande wa zawadi, ubora na viwango “Alisema.
Alisema mashindano hayo yatafanyika kwa siku mbili tarehe 12 na 13 mwezi ujao na kwamba yatakuwa mbio za kilomita 196 kwa wanaume, 80 kwa wanawake, upande wa walemavu ni Kilometa 15 kwa walemavu wanaume na Kilomita 10 kwa walemavu wanawake.
“Washindi katika kila kundi watapewa zawadi mbalimbali ambazo tutazitangaza baadaye,”Alisema.
Alifafanua kuwa mashindano ya mwaka huu ya Vodacom Mwanza Cycle Challenge yameandaliwa na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania kwa takribani miaka mitano sasa na kudhaminiwa na Alphatel, TBL, Knight Support na SBC kupitia kinywaji chake cha Pepsi.
Alisema Alphatel watadhamini mashindano ya walemavu, Knight Support watatoa ulinzi, huduma ya kwanza na gari la wagonjwa wakati SBC watakuwa wasambazaji rasmi kwa kupitia kinywaji chake baridi cha aina ya Pepsi .
“Shindano hili la Vodacom Mwanza Cycle Challenge ni mahususi kwa kukuza mchezo huu hapa nchini kwa lengo la kupata wawakilishi bora katika mashindano mbalimbali ya kimataifa,”alifafanua.
Alisema kampuni yake imekuwa ikidhamini michezo mbalimbali kama vile Soka, Riadha, kuogelea, mashindano ya boti, mashindano ya Mbuzi, Vodacom Miss Tanzania,Tenisi na mingine mingi ili kuhakikisha kwamba taifa linafanya katika tasnia nzima ya michezo.
No comments:
Post a Comment