Wednesday, October 13, 2010

TAARIFA KWA UMMA


Align CenterJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAHAKAMA YA TANZANIA

TAARIFA KWA UMMA


Taarifa hii ya uongozi wa Mahakama ya Tanzania ni kutokana na yaliyojitokeza leo siku ya tarehe 13 Oktoba 2010 nje ya jengo la Mahakama Kuu mara baada ya kesi Na. 95 ya Mwaka 2003 kuahirishwa. Uamuzi huo wa Mahakama ulipokelewa kwa hisia tofauti.Taarifa hii inakusudia kutoa ufafanuzi sahihi wa suala zima ili kuepuka tafsiri potofu inayoweza kujitokeza.

Ieleweke kuwa shauri la msingi lilikwisha Mahakamani kwa kutolewa hukumu ambayo ilitoa ushindi kwa Wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni Karata Ernest na Wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa mujibu wa sheria, ukazaji wa hukumu dhidi ya Serikali una matakwa yanayotakiwa kukidhiwa, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha maombi Mahakamani kwa ajili ya kuomba Hati (Certificate).

Hati hiyo huwasilishwa kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali (Paymaster General) kwa ajili ya taratibu za malipo (Kifungu cha 16 cha Government Proceedings Act Sura ya 5 ya Sheria kama zilivyorejewa mwaka 2002).

Washindi, pamoja na mambo mengine wamekuwa na mitazamo miwili tofauti kuhusiana na tuzo, idadi ya wanaodai na idadi ya wanaostahili kulipwa. Hii ni sababu kuu iliyochelewesha suala hili kufikia tamati. Hili ndio lililopelekea Mahakama kutoa amri tarehe 27 Julai 2010.

Tarehe 27 Julai 2010, Mahakama ilitoa amri kwa washindi kuwasilisha maombi ya pamoja baada ya kubaini kuwepo makundi hayo mawili yanayopingana miongoni mwao. Zaidi, tarehe hiyo Mahakama ilipanga kusikiliza maombi haya tarehe 27 mwezi Septemba 2010 baada ya kupokea nyaraka zote muhimu.

Kwa bahati mbaya, tarehe hiyo iliyopangwa maombi hayo hayakuweza kusikilizwa sababu Mh. Jaji N. M. Mwaikugile alikuwa katika likizo fupi. Lakini hata kama angekuwepo bado yasingeweza kusikilizwa sababu hakukuwa na Kiapo cha pamoja kwa Washindi (Joint Affidavit by the Decree Holders).

Hii ni kutokana na mawakili wanaowakilisha makundi haya mawili walihitaji muda zaidi wa kuhakiki orodha ndefu ya Wadai ili kuandaa kiapo hicho cha pamoja. Mawakili walikuwa na ombi la kuomba kuongezewa muda ili waweze kuwasilisha kiapo hicho.

Hii ilipelekea shauri hili kupangwa tarehe ya leo (13 Oktoba 2010) ambapo wangewasilisha maombi yao mbele ya Mh. Jaji anaesikiliza shauri hili.

Tarehe ya leo Mh. Jaji, ameamua kujitoa kuendelea na shauri hili ili haki itendeke na kuonekana imetendeka kwa mujibu wa taratibu na kanuni za kimaadili zinavyoelekeza.

Jalada liliwasilishwa mbele ya Mh. Jaji Kiongozi ambae alimpangia Mh. Jaji Utamwa. Leo hii, mawakili wa makundi yote mawili pamoja na Wakili wa Serikali wamewasilisha hoja zao mbele ya Mh. Jaji J.H.K. Utamwa kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha nyaraka muhimu. Mh Jaji amelikubali ombi hilo kwa kuwataka wahusika wawasilishe nyaraka hizo kabla au siku ya tarehe 15 Oktoba 2010 saa tano asubuhi. Shauri limepangwa kutajwa tarehe hiyo hiyo kwa ajili ya amri stahili.

Huu ndio ukweli wa suala hili na si vinginevyo. Ieleweke pia kuwa kama isingekuwa kutoelewana kwa washindi, suala hili lingekuwa limeshafikia tamati siku nyingi.


F.S.K. MUTUNGI

MSAJILI MAHAKAMA YA RUFAA

13 Oktoba 201

No comments:

Post a Comment