
Awali sharti kuu lilikuwa ni kuonyesha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na cheti cha kuzaliwa, lakini sasa wanaotaka kujiandikisha wamedai kuwa wanatakiwa kutaja nambari za nyumba, kuonyesha vyeti vya ndoa au kwenda na mke au mume, ili wakubaliwe kuingizwa kwenye daftari hilo.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Salim Kassim amethibitisha habari hizo akisema ni jambo la kawaida, lakini hajapata malalamiko ya mtu yeyote kudaiwa cheti cha ndoa.
Alisema Sheria ya Uchaguzi inasema mtu anatakiwa kupeleka vielelezo ambapo kwa mtazamo wake namba ya nyumba ni moja ya kielelezo cha mtu kutambuliwa ukaazi wake ikiwa atatiliwa shaka.
“Hili ni jambo la kawaida kaka yangu, wala halina wasiwasi, sheria inataka utoe vielelezo, kwa hiyo hata namba ya nyumba ni moja ya vielelezo,” alisema Kassim.
Kassim alithibitisha pia kutokea kwa mkanganyiko wa vituo kwa wananchi kati ya kile cha Karakana na cha Chumbuni, kwa maelezo kuwa imesababishwa na vituo hivyo vya shehia mbili tofauti kuwekwa kwenye shule moja.
Kutaka kuthibitisha hilo, Kassim alimkabidhi simu yake mtu aliyemtambulisha kuwa ni wakala wa CUF wa eneo la Chumbuni, Ali Hassan Haji ambaye aliiambia Mwananchi kuwa wanaotaka kujiandikisha wanaulizwa namba za nyumba, alikanusha kudaiwa vyeti vya ndoa.
Alisema mkanganyiko wa vituo unatokana na uamuzi wa kuligawa jimbo hilo na hivyo kuwafanya wananchi wameshindwa kujua wapo katika shehia au jimbo gani.
“Lakini tumeshalitatua wala halina tatizo,” alisema Haji.
Katika shehia za Chumbuni na Karakana zilizo kwenye jimbo la Chumbuni, Wilaya ya Mjini, Unguja, watu kadhaa walikataliwa kuandikishwa kwa madai kuwa si wakazi, licha ya kuwa na vielelezo vya msingi vya kupatiwa haki hiyo.
Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wananchi waliokataliwa walisema hata Zec imezidiwa nguvu na masheha na viongozi wa CCM wa jimbo hilo na hivyo kushindwa kuwasaidia wananchi.
Juma Mohammed mkazi wa Chumbini alisema ukipeleka nambari ya nyumba unayokaa, unaambiwa wewe ni wa Daraja Bovu Juu, ukienda Juu unaambiwa wewe ni mkazi wa Daraja Bovu Chini.
“Ili mradi tunahangaishwa tu... sheria haijasema kwamba tuchukue namba za nyumba, vyeti vya ndoa au mtu kuonyesha mume au mke wake kama sifa ya kuandikishwa,” alisema Mohammed.
“Ukiepeleka namba ya nyumba Karakana unaambiwa wewe ni mkazi wa Chumbuni, ukienda Chumbuni unaambiwa wewe ni mkazi wa Karakana, inakuwa sisi ni watu wa kuzungushwa tu hadi tunakosa haki zetu.”
Naye Juma Hamad, kutoka shehia ya Karakana, alisema waliwaambia na sheha wao kuwa hawezi kwenda kinyume na maagizo ya mkuu wa wilaya.
“Ukienda unaambiwa wewe ni mkazi wa Mto Pepo Juu, ukienda Juu unaambiwa wewe ni mkazi wa Mto Pepo Chini. Kwa kweli tunafanyiwa mizengwe ya kunyimwa haki zetu tu,” alisema Hamad.
No comments:
Post a Comment