RAIS wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela (Madiba) amelazwa katika hospitali ya Milpark mjini Johannesburg nchini humo kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
Hali hiyo imeleta tafrani kwa wakazi wa nchi hiyo ambao wameanza kupatwa na wasiwasi kuhusu afya ya kiongozi huyo aliyeongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi enzi za utawala wa makaburu.Mandela mwenye umri wa miaka 92, alipelekwa hospitalini hapo juzi usiku, hali iliyoibua hisia za wananchi huku vyombo vya habari vikifuatilia kwa karibu hali ya kiongozi huyo katika hospitali alikolazwa.
Serikali nchini humo imeimarisha ulinzi katika katika eneo la hospitali ya Milpark, na mamia ya wananchi wanazidi kumiminika katika eneo hilo wakitaka kujua afya ya Mandela ambaye alifungwa miaka 27 gerezani enzi za utawala wa mabavu wa makaburu.
Habari zinasema polisi walishika doria wakati msongamano wa magari ukiongezeka kwenye jengo lililoko mjini Johannesburg, huku waandishi wa habari wakiendelea kumiminika nje ya jengo hilo.
Mtalaka wa Mzee Mandela Winnie Madikizela-Mandela alibubujikwa machozi baada ya kumtembelea mumewe wa zamani hospitalini Milpark.
Winnie alionekana akifuta machozi machoni mwake na kisha kufuta pua yake wakati akitoka nje ya hospitali hiyo majira ya saa saba na nusu mchana jana.
Winnie alikuwa ameambatana na mjukuu mkubwa wa mzee Mandela, chief Mandla Mandela pamoja na wanafamilia wengine.
Mwanaharakati anayepinga ubaguzi wa rangi nchini humo, Albertina Sisulu alionekana mapema hospitalini hapo akiingia na kiti cha kusukumwa na baadaye akaondoka, lakini akiwa na tabasamu la matumaini wakati akipunga mkono kwa wapiga picha wa vyombo mbalimbali vya habari.
Waziri wa Sheria, Jeff Radebe, Mpambe wa mzee Mandela Zelda la Grange, na mtoto wa mke wa mzee Mandela Graca Machel nao walionekana hospitalini Milpark.
Maafisa wa ngazi za juu wa nchi hiyo pia walionekana katika viwanja vya hospitali hiyo.
Waandishi watatu kutoka shirika moja la habari nchini China waliomudu kujipenyeza katikati ya walinzi na kuingia ndani ya hospitali hiyo walikamatwa na kunyang'anywa kamera zao na askari polisi.
Vyombo vya habari vimezuiwa kuingia ndani ya hospitali na wanaweza tu kuona eneo la hospitali kwa kujiegesha katika daraja lililopo karibu na hospitali hiyo.
Kiongozi huyo mashuhuri anayejulikana na raia wengi Afrika Kusini kwa jina jingine la Madiba, afya yake imekuwa ikizorota na amekuwa hatokei hadharani mara kwa mara.
Idadi kubwa ya wanafunzi waliokuwa nje ya hosipitali ya Milpark wakionekana wenye huzuni, wamekuwa wakituma salamu za kumtakia heria Mzee Madiba.
Vyanzo vya habari kutoka nchini humo vinaendelea kusema kuwa, Mandela ni kawaida yake kwenda hospitali kuangalia afya yake, lakini zamu hii kilichowatisha ni Rais huyo kukaa hospitali hapo kwa muda mrefu.
Kutokana na wasiwasi uliotanda Ofisi ya Rais wa nchi hiyo iliwatahadharisha waandishi wa habari “wasiwasumbue madaktari wanaomtibu kiongozi huyo, na pia wahakikisha wanampa heshima anayostahili”.
"Rais Mandela afya yake ipo sawa, na kundi la watalaamu tayari wameiangalia afya yake,” ilisema sehemu ya taarifa kutoka ofisi ya Rais Yacob Zuma.
Ofisi ya Mandela pia ilitoa taarifa fupi kuutuliza umati wa watu waliojaza katika eneo na Milpark ikisema kuwa kiongozi huyo yupo hospitalini katika utaratibu wa kila siku kwa ajili ya kuchunguzwa afya yake na kwamba hakuwa na tatizo lolote kwani afya ni njema.
Hata hivyo msemaji wa Mandela hakuweza kutoa ufafanuzi kukidhi kiu ya wananchi waliotaka kufahamu zaidi kuhusu afya ya Rais huyo wa kwanza wa serikali ya kidemokrasia.
Mara ya mwisho kuonekana hadharani ilikuwa kwenye hafla ya kufunga mashindano ya Kombe la Dunia, yaliofanyika nchini humo mwezi Julai mwaka jana.
Aidha, chama kinachotawala nchini humo cha ANC kimesema hakuna haja ya kuwa na hofu kuhusu hali Mandela.
“Mandela ana umri wa miaka 92, kutokana na umri wake atapatwa na maradhi naombeni musiwe na hofu yoyote,” alisema msemaji wa ANC, Jackson Mthembu.
No comments:
Post a Comment