Monday, October 11, 2010

KAIJAGE APIGWA STOP NA TFF

Afisa habari wa TFF aliyesimamishwa kazi
Florian Rweyemamu Kaijage

Shirikisho La Mpira wa Miguu nchini (TFF) limemsimamisha kazi afisa habari wake, Florian Kaijage (pichani) kutokana na fedheha ya kushindwa kutimiza itifaki muhimu ya kupiga nyimbo za taifa wakati wa mechi ya Taifa Stars na Morocco jumamosi jijini.

Rais wa TFF Sir Leodegar Chilla Tenga amewaambia waandishi wa habari jijini Dar leo kuwa tukio hilo ni la aibu mbele ya Rais Jakaya Kikwete, mashabiki na wageni wengine na mbaya zaidi kwa vile mchezo huo ulionyeshwa katika luninga ndani na nje ya nchi, hivyo aibu hiyo imeshuhudiwa na wapenzi wa soka kote duniani.

Amesema TFF imemua kumwajibisha Kaijage kwa kuwa ndiye aliyekuwa amepewa jukumu la kusimamia jambo hilo. Aidha alisema wakati amesimamishwa kaijage ataisaidia timu itakayoundwa kuchunguza jambo hilo na kuongeza kuwa hatua zitachukuliwa kwa yeyote Yule atakayebainika kuhusika kwa tukio hilo.

Amesema jambo hilo halikustahili kutokea kwa kuwa liliishawahi kutokea wakati wa mchezo na Brazil ambapo safari hii wahusika walipewa jukumu la kuhakikisha kuwa wanazijaribu nyimbo zote siku mbili kabla ya mchezo na kuhakikisha kuwa hakuna hitilafu yoyote na wahusika walimuhakikishia kuwa hakutatokea dosari yoyote.

“Kushindwa upigaji nyimbo za taifa ni upungufu mkubwa kiutendaji na kama nilivyosema hapo awali ni aibu kwa taifa letu, napenda kwa niaba ya tff kuomba radhi kwa Mheshiwa Rais, wapenzi waliofurika uwanjani, Watanzania kwa jumla na wageni wetu kutoka Morocco” alisema tenga.

Alisema kuanzia sasa, hata kama mitambo ya uwanjani ni mizima, patakuwepo bendi za police/jeshi ama mitambo ya tahadhari kwa ajili ya nyimbo za taifa na matangazo mengine muhimu.
Aidha, wadau wengi wa soka, ikiwemo waandishi wa habari za michezo, wamefurahishwa na hatua hiyo, na wengi wameipongeza TFF kwa kuchukua hatua hiyo kwa kile walichodai kwamba hilo ni fundisho kwa waliopo na wataokuwepo baadae.
Hii si mara ya kwanza kwa Kaijage 'kukanyaga nyanya' ikikukmbukwa kuwa siku Brazil walipocheza na Taifa Stars uwanja huo huo wa Taifa, na mbele ya JK, kwenye luninga la uwanjani kulioneshwa picha za mafaili ya kazi badala ya kinachoendelea uwanjani. Pia nyimbo za Taifa za nchi hizo zilipatwa na kwikwi na badala yake zikasikikika ngoma za sindimba.
Kabla ya mechi na Morocco waandishi wa habari za michezo kupitia chama chao TASWA nusura wasusie kuandika habari za TFF kutokana na utata wa kuingia uwanjani, kinara kwa upande wa TFF akiwa Kaijage ambaye pia amekuwa akilaumiwa kufanya kazi zisizomhusu kana kwamba yeye ni Katibu mkuu na sio afisa habari.

No comments:

Post a Comment