Thursday, May 6, 2010

MKUTANO WA UCHUMI KWA AFRICA UNAENDELEA DAR








Mh Dk Jakay Mrisho Kikwete akiwa na Mh. Klaus Schwab, mwasisi na mwenyekiti wa World Economic Forum wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 20 wa Uchumi wa Dunia kwa Afrika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar jana.

MH RAIS ALIA NA MALARIA KWENYE UFUNGUZI.

RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa ni bora Tanzania kukosa mapato, kuliko kupoteza maisha ya maelfu ya Watanzania wanaokufa kwa ugonjwa wa malaria.

Rais Kikwete aliyasema hayo leo kwenye mkutano wa Uchumi Duniani (WEF), unaowakutanisha washiriki kutoka nchi 85 duniani ambapo pamoja na mambo mingine unajadili namna ya kunyanyua uchumi wa Bara la Afrika hasa baada ya kukumbwa na msukosuko wa uchumi duniani mwaka mmoja uliopita.

Hata hivyo, mkutano huo unakusudia kutoa changamoto na mapendekezo ya njia sahihi ya kupambana na kutokomeza kabisa ugonjwa huo namba moja kwa kusababisha vifo vya kina mama waja wazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano duniani.

Katika kipindi cha maswali na majibu ya papo kwa hapo baina ya washiriki wa mkutano huo, Rais Kikwete alieleza mikakati mbalimbali ya kutokomeza malaria nchini.

Moja ya mikakati hiyo ni kwa serikali kuzifutia ushuru bidhaa zote zinazohusiana na matibabu pamoja na mapambano dhidi ya malaria kuingia nchini, jambo ambalo baadhi ya Watanzania wanadhani huenda likaathiri pato la taifa.

Lakini Rais Kikwete akionekana mwenye furaha baada ya Tanzania kumwagiwa sifa katika mkutano huo kutokana na juhudi zake za kupambana na malaria.

“Lakini kama kuna maelefu ya Watanzania wanapoteza maisha kwa sababu ya malaria na tunaweza kuyaokoa basi ni afadhali tukose mapato, lakini tuokoe maisha ya Watanzania,”alisema Rais Kikwete.

Alisema licha ya mapambano dhidi ya malaria kuanza kwa muda mrefu nchini, lakini serikali yake inaona ndio kwanza yanaanza kutokana na umuhimu na haja kubwa iliyopo ya kutokomeza ugonjwa huo na hatimaye kuokoa maisha ya nguvu kazi ya Watanzania.

No comments:

Post a Comment