Monday, April 18, 2011

Slaa anatumiwa - CCM.


CHAMA Cha Mapinduzi kimesema Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na chama chake, wanatumiwa na baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi waliotakiwa kujiuzulu wenyewe ndani ya chama hicho.

Akihutubia umati wa watu katika viwanja vya Mwembe-Kisonge Zanzibar, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema kwa sasa watuhumiwa hao wameamua kutumia baadhi ya vyama vya siasa, magazeti na asasi za dini kujibu mapigo.

“Tumewapa miezi mitatu watuhumiwa wote wa ufisadi katika chama chetu wajiondoe wenyewe. Baadhi wanajaribu kupinga na kujibu mapigo kwa kutumia magazeti, vyama vya siasa na taasisi za dini...tunajua tutashinda na wao lazima waondoke,” alisema Nnauye.

Alisema, “Tumeandaa mkakati wa kusafisha chama kutoka ngazi za chini mpaka katika ngazi ya Taifa. Tumechunguza na tunajua wanaotakiwa kuondoka ndani ya chama chetu. Lakini baadhi ya watu wamejitokeza kutaja majina ya watuhumiwa ndani ya chama chetu, hiyo si kazi yao.”

Aprili 16 Dk. Slaa akiwa mkoani Tabora, aliwatuhumu baadhi ya viongozi wastaafu wa CCM na waziri mmoja kuwa miongoni mwa aliowaita orodha mpya ya watuhumiwa wa ufisadi.

Lakini Katibu huyo wa Chadema, alifanya hivyo siku chache baada ya CCM katika mkakati wake wa kujivua gamba, kuwataka watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho kujiuzulu wenyewe ndani ya miezi mitatu ijayo kabla ya kuondolewa kwa nguvu na Halmashauri Kuu ya
Chama hicho Taifa (NEC).

Dk. Slaa alifanya hivyo akijua kuwa sekretarieti mpya ya CCM, ikiwa na viongozi wapya imeanza ziara kutambulisha uongozi mpya kwa wanachama wake na kuelezea uamuzi mgumu wa kujivua gamba walioufanya mkoani Dodoma.

Naye Katibu wa Itikadi, Siasa na Ushirikiano wa Kimataifa, January Makamba alisema wamejipanga kufanya mageuzi makubwa kwa ajili ya kukiendeleza chama hicho na Taifa na kuahidi kuwa mabadiliko hayo yatamfurahisha kila mmoja.

Pia Naibu Katibu Mkuu, Tanzania Bara John Chiligati alisema mabadiliko yaliyofanyika hivi karibuni, yanalenga kuokoa chama hicho kutokana na hali ya kupoteza kukubalika kwake kwa jamii.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai aliwataka wanachama kujitolea kujenga chama hicho, ikiwa ni pamoja na kuacha migogoro ya makundi ndani ya chama hicho na kujenga umoja.

Kabla ya viongozi hao kuzungumza na wapenzi wa chama hicho, Katibu Mkuu wa mpya wa CCM, Wilson Mukama aliwaambia wafuasi wa chama hicho kwamba Sekretarieti mpya
imejitoa kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho.

Mapema kabla ya kuwatambulisha viongozi wapya katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa, alisema wamefanya mabadiliko katika kanuni za chama hicho, ili Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar awe Mjumbe wa NEC kutokana na nafasi yake badala ya Waziri Kiongozi ambaye nafasi hiyo kwa sasa haipo.

Msekwa alieleza sababu zilizosukuma chama hicho kufanya mabadiliko hayo kwa lengo la kurudisha kukubalika kwake kwa wananchi na wanachama wake.

“Huku ni kuzaliwa upya baada ya Februari 1977 wakati Tanu na ASP zilipoungana,” alisema Msekwa.

Akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho na wananchi waliojitokeza kuwakaribisha viongozi hao, Msekwa alisema matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita yalikuwa ishara ya wazi kwamba chama kilianza kupoteza mvuto wake kwa wananachi.

Alisema hali hiyo ilisababaisha Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuunda Kamati Maalumu ya watu sita ikiongozwa na Mukama ambaye aliwaaalika wataalamu (ambao si wanachama wa CCM) kutafuta mzizi wa tatizo hilo.

Kamati hiyo kwa mujibu wa Msekwa, ilieleza kuwa CCM imebebeshwa mzigo wa kuwa na baadhi ya wanachama wake ambao wanatuhumiwa na wananchi kwa kuhusika katika rushwa.

Alisema kutokana na mzigo huo, CCM ilichafuka kwa kuonekana chama cha walarushwa na mafisadi.

No comments:

Post a Comment