Monday, April 18, 2011

Yaliyojiri kwa Babu!


MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, wameutaka uongozi wa wilaya hiyo kuruhusu Halmashauri yao kuanza kukusanya ushuru kwa magari yote yanayopita wilayani hapo kupeleka wagonjwa Loliondo kwa Mchungaji Ambilikile Mwaisapile.

Madiwani hao waliazimia kutozwa kwa ushuru huo wakati wa kikao cha bajeti cha Halmashauri hiyo ambacho kiliongozwa na Mwenyekiti wao, Joseph Malimbe.

Madiwani hao waliazimia kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Francis Isaac, ili washirikiane kuandaa utaratibu wa kukusanya ushuru wa magari kutoka katika kituo hicho cha Kanda ya Ziwa.

Walisema ushuru huo utasaidia kuboresha usafi na kuweka miundombinu mizuri katika kituo hicho ambacho kimekuwa kikipokea magari mengi kutoka mikoa yote ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kupeleka wagonjwa katika kijiji cha Samunge kupata kikombe cha Mchungaji huyo maarufu Babu.

“Tutazungumza na Mkuu wa Wilaya yetu, maana wote ni Serikali, tuzungumze namna ya kukusanya ushuru kwenye kituo hicho...na ushuru huu utasaidia kuboresha usafi na kuboresha miundo mbinu,” alisema Malimbe.

Kwa sasa kila gari inayopita katika kituo hicho, imekuwa ikitozwa Sh 1,000 tu, kwa ajili ya kibali cha kuruhusiwa kwenda huko Loliondo.

Wakati huo huo, Lucas Raphael anaripoti kutoka Tabora kuwa uongozi wa mkoa huo umeweka utaratibu wa wananchi kwenda kunywa dawa kwa Babu kupitia kituo cha Kanda ya Kati.

Kwa mujibu wa utaratibu huo, Jumatatu, Jumanne na Jumapili watapita watu wenye magari madogo na Jumatano, Alhamisi na Jumamosi zitakuwa kwa wasafiri wanaotumia mabasi.

Akitoa utaratibu huo jana, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Abeid Mwinyimsa alisema uamuzi huo umefikiwa wakati wa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Alisema kila mwenye basi atachukua watu wasiozidi 60 kwa siku moja huku akisisitiza wagonjwa mahututi wasipelekwe.

Mwinyimsa alisema uongozi wa Mkoa umeweka utaratibu wa kila mwenye gari dogo au basi kupata kibali cha muda cha kuwapeleka watu huko kwa kupitia kituo cha Babati ambacho kinachotumiwa na mikoa ya Singida, Dodoma, Tabora, Manyara pamoja na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mwinyimsa alisema Ofisi ya Waziri Mkuu imeweka utaratibu wa Kanda tatu kwa ajili uthibiti wa usafirishaji wa abiria kwenda Loliondo ikiwemo Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini pamoja na Kanda ya Kati.

Alisema kuwa Tabora imepangiwa kupeleka watu wasiozidi 60 kila siku kwenda kunywa dawa ya Babu huko Samunge na kuwataka wote wanaotaka kwenda Loliondo kujiandikisha kwenye ofisi za wakuu wa wilaya wanakotoka badala ya kila mmoja kuondoka apendavyo.

Alisema ofisi za wakuu wilaya zitawasilisha majina kwa Katibu Tawala wa Mkoa ili waratibu idadi ya watu wa mkoa mzima wanaokwenda Babati kila siku, ili wapate vibali vya magari husika bila kuchelewa.

Alisema kila gari linalokwenda Loliondo litatozwa Sh 5,000 katika kituo cha Yamimdito na wataokusanya tozo hiyo ni Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

No comments:

Post a Comment