Thursday, November 18, 2010

SERIKALI YAANZA KUBORESHA MICHEZO KATIKA VYUO VYA UALIMU


Mkurugenzi Mafunzo ya Ualimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi. Rose Massenga akiongea na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika leo katika ofisi za wizara hiyo.


NA VERONICA KAZIMOTO- MAELEZO

Zaidi ya shilingi milioni 800 zinatarajiwa kutumika katika mradi wa kuboresha Elimu kwa Michezo katika vyuo vya ualimu kumi na moja hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa Habari Mkurugenzi Mafunzo ya Ualimu Rose Massenga amesema fedha hizo zimetolewa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la LiiKE la Finland ili kufanikisha mradi huu.

“Mradi huu unalenga kuandaa walimu 300 kila mwaka kwa muda wa miaka 3 ambao watafundisha somo la Elimu kwa Michezo katika shule za misingi, sekondari na vyuo vya ualimu ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati endelevu baada ya kipindi cha mradi.” Massenga amesema.

Massenga amefafanua kuwa lengo la mradi huu ni kupata walimu wenye uwezo na sifa za kufundisha somo la Elimu kwa Michezo ili kupata vijana wenye vipaji watakaoweza kuonesha uwezo wao na hatimaye kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa.

Kwa sasa vyuo hivyo vimeshapewa vifaa vya Michezo, vitabu vya elimu kwa Michezo kwa kila chuo, mipira 825 ya Michezo mbalimbali, kukarabati Ofisi ya Elimu kwa Michezo pamoja na stoo.

Vifaa vingine vilivyonunuliwa ni gari na kompyuta nne kwa wafanyakazi wa mradi, kompyuta za mezani 11 na vifaa vyake pamoja na kukarabati viwanja vya Michezo. Pia wakufunzi 2 wameteuliwa kufundisha Michezo katika vyuo hivyo.

Masenga amevitaja vyuo hivyo kuwa ni mtwara kawaida, mtwara ufundi, korogwe, ndala, kasulu na monduli. Vingine ni mpwapwa, tarime, songea, ilonga na kireluu.

No comments:

Post a Comment