HALMASHAURI kuu ya CCM imetoa ratiba ya mchakato wa kupata wagombea wake katika uchaguzi mkuu ujao huku mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete akitamba kuwa ni lazima chama hicho tawala kipate tena ushindi wa kishindo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na chama hicho tawala, wagombea urais watakaopitishwa na CCM, ambao ni mgombea wa urais wa Muungano na rais wa Zanzibar, watatangazwa Julai 17 mwaka huu.
Ratiba hiyo imeonyesha kuwa majina ya wagombea wa nafasi hizo za urais, yatapendekezwa Julai 16 mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, iliyochapishwa kwenye kitabu kidogo chenye kichwa cha habari 'Ratiba ya Namna ya Kuwapata Wagombea wa Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani Watakaogombea katika Uchaguzi Mkuu wa Dola mwaka 2010", ilijadiliwa na kupitishwa katika mkutano mkuu wa halmashauri kuu uliomalizika juzi jijini Dar es Salaam.
"Julai 10 mwaka huu, kamati maalum ya halmashauri kuu ya taifa ya Zanzibar na sekretarieti ya halmashauri kuu ya taifa ya CCM itakaa kujadili waombaji wa nafasi ya urais wa Muungano Julai 12 hadi 14 mwaka huu," kinaeleza kitabu hicho.
Taarifa hiyo inafafanua kuwa mkutano mkuu maalum wa CCM utafanyika kuteua jina moja la mgombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julai 17 mwaka huu.
“Baada ya hapo wagombea wadhaminiwa na wapigakura mikoani kwa mujibu wa tarehe zitakazowekwa na Tume ya Uchaguzi (Nec) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec),†inafafanua taarifa hiyo.
Kuhusu uteuzi wa wagombea wa nafasi ya ubunge na ujumbe wa baraza la wawakilishi ratiba imeonyesha kuwa fomu zitolewa Julai 26 hadi Julai 28 mwaka huu.
Mikutano ya kampeni za wagombea hao ndani ya chama, itaanza Julai 29 na kuendelea hadi Agosti 7 mwaka huu, huku kura za maoni kwa wagombea hao zikipangwa kufanyika Agosti 8.
Ratiba imeonyesha kuwa matokeo ya kura hizo yataandaliwa Agosti 9 hadi Agosti 10 mwaka huu na Agosti 11 kamati za siasa wilaya zitakutana kuwajadili wagombea ubunge na uwakilishi kabla ya kamati za siasa za mikoa kujadili majina hayo na kutoa mapendekezo kwa kamati kuu.
“Kamati maalum ya halmashauri kuu ya taifa ya Zanzibar, itawajadili wagombea wa ubunge na uwakilishi wa majimbo na viti maalum wanawake Agosti 15, sekretarieti ya NEC itawajadili Agosti 16 hadi 17 na kamati kuu itapendekeza majina ya wagombea Agosti 18 na 19 mwaka huu,†inaeleza ratiba hiyo.
Kuhusu uteuzi wa wagombea udiwani wa Bara na Zanzibar, fomu zitachukuliwa Julai 26 na kurudishwa Julai 28 mwaka huu.
Akizungumza kwenye kikao cha wajumbe wa halmashauri kuu ambacho pia kilijumuisha wenyeviti na makatibu wa mikoa, Rais Kikwete alisema CCM ni lazima iibuke na ushindi wa kishindo mwaka huu.
"Tutaangalia uwezekano wa kuwatumia vijana wetu na makada wetu watakaokuwa tayari kujitolea kufanya kazi za chama wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi ili wasaidie shughuli mbalimbali kwenye ofisi za wilaya, mikoa na makao makuu," alisema Kikwete.
Alitaja nyenzo za ushindi huo kuwa ni kueleweka kwa agenda na ujumbe kwa wanachama, kuwa na wagombea makini na wanaokubalika, na kuwa na vifaa vya kuendeshea kampeni.
Kwa mujibu wa Kikwete, ambaye anatarajiwa kutetea nafasi yake ya urais wa Jamhuri ya Muungano aliyoipata mwaka 2005, chama hicho kimetoa magari katika wilaya zote nchini na kwamba sasa kinajipanga kupata magari kwa ajili ya mikoa pia.
Kikwete, ambaye alisema idadi ya wanachama wa CCM inaongezeka kwa kasi na kwamba hivi sasa wanachama wamefika zaidi ya milioni 5, aliwakemea wenyeviti na makatibu waliohudhuria mkutano huo kwa kile alichokiita ni kutoa kadi za uanachama vichochoroni.
“Wapo watu ambao hawastahili kupewa kadi za chama, lakini wanapewa kwa njia za mkato.Kutolea kadi vichochoroni kunaonyesha njaa kubwa kwa makatibu na hili ni kosa kubwa,†alisema Kikwete.
Rais pia aliwakejeli watu wanaosema CCM ni ya watu wanye fedha na kusema kuwa chama hicho kinahitaji mtu atakayeweza kukiletea ushindi na siyo kuwa mzigo kwake.
“Watu wanasema CCM bila hela huwezi kushinda, lakini ukweli tunataka mtu anayekubalika na wananchi, yaani anayeweza kuifanya CCM ishinde, mambo ya fedha ni wao," alisema Kikwete.
Katika mkitabu hicho cha maelekezo kwa wagombea, kila mwanachama wa chama hicho ametakiwa kuungana na kushikamana kuhakikisha ushindi huo unapatikana.
“Kila mmoja katika mazingira anayoishi, aendelee kukisemea, kukipigania na kukipigia debe chama chetu ili tupate ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
"Naamini kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake, tutapata ushindi mnono pengine hata kuliko ule wa 2005,"alisema Kikwete.
"Tuendelee kuhimiza umoja, moyo wa upendo na mshikamano miongoni mwa viongozi wa CCM, wana-CCM, wapenzi na Watanzania kwa ujumla. Tumeshinda sana katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji. Lazima tushinde uchaguzi mkuu ujao. Kauli mbiu yetu mwaka huu ni, Ushindi mwa 2010 ni Lazima."
Katika kikao hicho, halmashauri kuu ya CCM pia ilitoa mwongozo kwa wanachama wake kuunga mkono serikali ya mseto.
Katika kuonyesha dhamira ya chama kuleta maelewano baina ya wafuasi wa CCM na CUF Zanzibar, Nec imetoa mwongozo kwa wana-CCM Zanzibar unaosisitiza umuhimu wa kuunga mkono pendekezo la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa visiwani humo,inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu kuundwa au kutoundwa kwa serikali hiyo uko mikononi mwa Wazanzibari.
Katika hatua nyingine Nec imempitisha jina la Amina Nassor Makilagi kukaimu nafasi ya Husna Mwilima ambaye aliondolewa kwenye wadhifa wa katibu mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM.
Kwa mujibu wa katiba ya UWT jina la Makilagi litapigiwa kura na baraza kuu la umoja huo, ili achaguliwe kushika rasmi wadhifa huo, inafafanua taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment